Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuthibitisha dhamira yake ya kumaliza tatizo la maji nchini kwa kuendelea kuwekeza fedha nyingi na usimamizi mahiri. Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuhakikisha wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini na mijini wanapata huduma bora zilizo endelevu ya maji safi na salama.
Kwa upande wa vijijini, serikali ya awamu ya Sita (6) chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejiwekea lengo la kufikia zaidi ya asilimia 85 ya uhakika wa upatikanaji wa huduma ya maji itakapofikia mwaka 2025.
Ili kufikia lengo hilo kubwa, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan inafanya jitihada za kujenga na kukarabati miradi ya maji pamoja na kupanua mitandao ya kusambaza maji na kuimarisha usimamizi wa huduma za maji vijijini. Kwa kipindi cha miaka mitatu Rais Mh. Dkt. Samia alichohudumu madarakani, jitihada na mikakati yake imewezesha kuongezeka kwa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kutoka wastani wa asilimia 77 kwa mwezi Desemba mwaka 2022 hadi kufikia wastani wa asilimia 79.6 iliyoripotiwa mwezi Desemba mwaka 2023.
Kiwango kilichoongezeka kimetokana na kutekelezwa kwa miradi 632 yenye vituo vya kuchotea 7,956 vyenye uwezo wa kuhudumia wananchi 4,740,959. Uwekezaji huu mkubwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, unafanya jumla ya wananchi wa vijijini wanaopata huduma ya maji kufikia 34, 950,368 kati ya wananchi 39,232,999 waishio maeneo ya vijijini kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ua mwaka 2022.
Kwa upande wa mijini, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, vivyo hivyo, ameongoza jitihada za makusudi za Serikali kupitia wizara na wadau mbalimbali wa maendeleo, kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo ya mijini.
Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mkazo wa mikakati ya kujenga, kukarabati na kupanua miradi ya maji, kwa lengo la kufikia zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wa mijini, kufikia mwaka 2025.
Matokeo ya kazi kubwa anayofanya Rais Dkt. Samia, yamewezesha kufikia lengo kwa wastani wa asilimia 90 ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo ya mijini, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 88 katika kioindi kama hicho mwaka 2022.
Ongezeko hilo limetokana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa bajeti kubwa ya fedha iliyowezesha kukamilisha miradi 85 ya maji inayohudumia wakazi 4,641,505 waishio maeneo ya mijini.